Sunday, June 12, 2016

Kongwa: Mama wa Majeshi ya Nchi za Afrika ya Kusini na Kati

Kongwa: Mama wa Majeshi ya Nchi za Afrika ya Kusini na Kati
Kama tunaweza kuandika orodha ya kambi kumi muhimu kihistoria za kijeshi Afrika nzima, naweza kusema bila kusita Kongwa itakuwepo kwenye orodha hiyo. Hata kama sisi tukilala usingizi na historia yetu, viongozi wa nchi za Afrika kamwe hawatasahau Kongwa. Hakuna viongozi wengi wakubwa wa majeshi ya nchi za Afrika ya kusini sasa hivi ambao hawakuguswa kwa namna moja au nyingine na Kongwa. Kongwa ina historia muhimu sana sio tu kwa Tanzania, bali kwa Afrika nzima. Hii ni moja ya sehemu ya historia inayotupa nafasi ya kujivunia kama watanzania. Mchango wa Tanzania katika harakati za ukombozi wa Afrika ni mkubwa sana. Kambi ya wanajeshi ya Kongwa, Dodoma, inatupa mfano mmoja wa namna Tanzania ilijitolea ili wengine wapate uhuru.
Mnamo mwaka 1964, serikali ya Tanganyika (Tanzania baada ya 1964) ilitoa sehemu ambayo ilifanywa shamba na serikali ya kikoloni iwe kambi ya wanajeshi. Kutokana na msimamo wa serikali ya Tanganyika chini ya uongozi wa Nyerere, Kawawa, Kambona na wengine, nchi za Afrika ziliamua Tanganyika iwe makao makuu ya Kamati ya ukombozi wa nchi za Afrika ya OAU mnamo mwaka 1963. Uamuzi huu ulionyesha jinsi gani Tanganyika ilikubalika kama nchi inayojali na kusaidia harakati za uhuru. Uamuzi ulifanywa na serikali ya Tanganyika kufungua kambi ya wanajeshi Kongwa. Kambi hiyo ilikuwa itumike kutoa mafunzo ya kijeshi kwa watu kutoka nchi za Africa.
Chama cha Namibia, SWAPO, kilipeleka watu wake kwenye kambi ya Kongwa. Kuanzia mwaka 1962, Sam Nujoma alifanya makubaliano na serikali ya Tanganyika ili wanamibia 200 waliojitolea waje Tanganyika, na kutoka hapo, waende nchi nyingine kwa mafunzo ya kijeshi. Wendi wao walienda Egypt kupata mafunzo hayo. Wengine walipelekwa Algeria mwaka 1963. Wengi wao walienda Kongwa walipomaliza mafunzo yao. Wanajeshi wa kwanza kutoka Namibia kwenda Kongwa walifika mnamo April 1964. Waliendelea na mazoezi na mafunzo ya kivita Kongwa. Waliohitimu walianza kufundisha wengine walioletwa moja kwa moja kutoka Namibia. Mnamo mwaka 1965, vijana sita waliopata mafunzo ya kivita walirudi Namibia kwa siri na kuanza opereshini ya ukombozi. Miungoni mwao alikuwa Simeon Tshihungeleni na Johannes Otto Nankudhu. Mnamo mwezi Agosti 1966, kundi lingine lilipenya na kuingia Namibia. Hilo lilikuwa kundi la kwanza kufyatua risasi ndani ya Namibia Agosti 1966; wengi katika kundi hilo walikua Kongwa na silaha walizotumia walizipata Tanzania.
Wanajeshi kutoka Mozambique walianza kuingia Kongwa mwezi Aprili 1964. Katika kundi la kwanza kuja Kongwa alikuwepo Samora Machel. Samora Machel alikuwa ni mmoja wa vijana waliopita Tanganyika mwanzoni wa mwaka 1963 kwenda kupata mafunzo ya kijeshi Algeria. Yeye na wenzake walikuwa miungoni mwa watu wa kwanza kuingia Kongwa na kuanza kuijenga kambi hiyo. Wanajeshi wa FRELIMO na SWAPO waliungana pamoja na kuanza kukarabati jengo la shule na kulifanya jengo la kambi. Pia waliweka senyenge kutenganisha kambi ya FRELIMO na SWAPO. Ikumbukwe kwamba chama cha FRELIMO kilianzishwa Dar es Salaam hapo awali mwaka 1962 baada ya Mwalimu Nyerere kuwaambia viongozi wa vikundi mbali mbali lazima waungane au waondoke Tanganyika.
Ilipofika mwezi wa Mei mwaka 1964, wanajeshi wa SWAPO na FRELIMO wakatoka kwenye matenti na kuingia kwenye kambi mpya waliojenga: Kongwa. Ni muhimu kukumbaka kwamba pamoja na serikali ya Tanganyika kujitolea sehemu hio iwe kambi ya kijeshi, wananchi wa maeneo ya Kongwa walijitolea sana kwa hali na mali kusaidia wanajeshi hao mwanzoni.
Kwa upande wa FRELIMO, kulikuwa na wanajeshi zaidi ya 250 ilipofika mwishoni wa mwezi Septemba 1964. Kundi la kwanza lilipenya kutoka Tanganyika na kuingia Msumbiji kaskazini mwanzoni wa Septemba 1964. Risasi na bunduki walizotumia walizipata Tanganyika. Silaha hizo zilitolewa na nchi tofauti na zikakabidhiwa serikali ya Tanganyika ili iwape wapiganaje wa nchi za Afrika. Huu ndio ulikua mwanzo wa vita vya kukomboa Msumbiji. FRELIMO iliondoa wanajeshi wake Kongwa na kuwapeleka kambi nyingine baada ya mwaka 1966; Nachingwea ikawa kambi kubwa na muhimu ya FRELIMO.
Chama cha African National Congress (ANC) cha Afrika Kusini kilipeleka baadhi ya watu wake wa kwanza waliojitolea kupigana Kongwa.ANC iliita jeshi lake Umkhonto we Sizwe (MK). Watu kutoka Afrika Kusini walianza kuingia Tanganyika kwa wingi kuanzia mwaka 1962. Wengi walipitia Tanganyika wakati wanaenda kupata mafunzo ya kivita, mwanzoni China na watu wachache, na baadae Urusi. Lakini ilikuwa mnamo mwaka 1963 ambapo wengi wao walipita Tanganyika na kwenda Urusi kwa mafunzo. Walianza kurudi Tanganyika mwaka 1964 baada ya kufudhu mafunzo. Ni muhimu kukumbusha kwamba hata hizo safari za kwenda nchi nyingine kupitia Tanganyika, ziliwezeshwa kwa kupitia hati za kusafiri walizopewa na serikali ya Tanganyika. Hili lilifanywa sio tu kwa Afrika Kusini, bali hata nchi nyingine za Afrika. Baadhi ya wanajeshi wa MK wa Luthuli Detachment waliopigana Wankie Kampeni kule Zimbabwe pamoja na ZAPU mwaka 1967, walikua Kongwa. Chris Hani alikuwa ni mmoja wa wanajeshi wachache waliofanikiwa kutoraka maadui katika opereshini hio na kukimbia Botswana.
Vyama kutoka Angola na Zimbabwe vilipeleka wapiganaji wake Kongwa. Chama cha MPLA cha Angola kilipeleka wanajeshi wake Kongwa mnamo mwaka 1965. MPLA ilitumia Kongwa kama sehemu ya kutoa mafunzo ya kivita kwa wanajeshi wake. MPLA haikuwa na wanajeshi wengi Kongwa. Pamoja na hayo baadhi ya wapiganaji wa kwanza wa MPLA waliofungua uwanja mpya wa mapambano Angola eneo la mashariki mwaka 1965 walikua Kongwa na baadae Zambia. Hata wanajeshi wa UNITA, walikua 11, walikaa Kongwa na wanajeshi wa SWAPO mwaka 1965 baada ya kufudhu mafunzo yao China.
Wapiganaji wa Zimbabwe wa chama cha ZAPU ni miungoni wa wanajeshi waliofika Kongwa mwaka 1965. ZAPU haikua na wanajeshi wengi Kongwa; wanajeshi hao walihamishwa na kupelekwa Zambia. Baadhi ya wanajeshi hao walipigana pamoja na MK kwenye Wankie Kampeni ya mwaka 1967 Wanajeshi wa ZANU pia walikuwepo Kongwa. Lakini wanajeshi wa ZANU baadae walipelekwa kwenye kambi ya Itumbi iliyopo Chunya, Mbeya.
Kongwa ni muhimu kwasababu ilitoa nafasi kwa wanajeshi kutoka nchi tofauti za Afrika kusini na kati kupata sehemu ya kufanya mafunzo na mazoezi ya kivita. Lakini pia, Kongwa ni muhimu kwasababu ilitoa nafasi kwa wanajeshi kutoka sehemu tofauti za Afrika kubadilishana mawazo na kupata kujuana. Pia hata wanajeshi waliotoka nchi moja, wengi walikua wanatoka makabila tofauti; Kongwa iliwapa nafasi ya kujifunza kujiunga pamoja. Kwa mfano, watu wa makabila tofauti kutoka Namibia walijikuta wanaisha pamoja sehemu moja na hivyo kulazimika kujifunza kuishi pamoja na kusaidiana.
Huu ni wakati muafaka kujikumbusha mchango mkubwa uliotolewa na Tanzania kusaidia harakati za ukombozi wa Afrika. Kuna mengi tunaweza kuongeza tunapoongelea mchango wa Tanzania, lakini kambi ya Kongwa ni mfano mmoja mzuri unaoonyesha mchango mkubwa uliotolewa na serikali na wananchi wa Tanzania. Na pia tukumbuke kwamba Kongwa haikuwa peke yake; baadae kambi nyingine zilifunguliwa Mgagao, SOMAFCO, Nachingwea, Bagamoyo, na Itumbi. 
Mchango wa Tanzania katika harakati za ukombozi wa Africa ni mkubwa sana. Hili ni jambo moja linalotakiwa kumfanya kila Mtanzania ajisikie ufahari mkubwa. Na kwa kutoa mchango huu, tukumbuke kwamba Tanzania iliadhibiwa sana kiuchumi na kwa namna nyingine. Lakini hilo halikututingisha; tulisimama imara kama nchi na kuhakikisha zile haki za binadamu, kama uhuru, haukanyagwi. Leo hii tunaweza kusema kwa tabasamu kubwa kwamba Kongwa ilikuwa ni mama wa majeshi tunayoyaona nchi za kusini mwa Afrika na kati.
Aluta Continua!
Azaria Mbughuni
Azmbughuni@gmail.com





No comments:

Post a Comment