Tuesday, May 7, 2019

Mtemi Kibete: Shujaa wa Kinyamwezi


Tanzania ina mashujaa wengi katika historia yake. Mashujaa wengi wanasahaulika jinsi muda unavyozidi kupita. Ingawa wakina mama walipata nafasi kubwa za kuchukua uongozi na kufanya kazi kubwa kupinga ukoloni, ni wachache sana wanakumbukwa kwa uongozi wao au jitihada zao katika harakati za kupinga utawala wa kikoloni. Mmoja ya mashujaa hao ni Mtemi Kibete wa Unyamwezi. Historia ya maisha ya Mtemi Kibete inatufundisha mengi kuhusu maisha yake na historia ya Tanzania, tunajifunza kuhusu baba yake Chifu Mirambo alikuwa ni mtu wa aina gani, na tunajifunza kuhusu ujasiri wa kina mama, nafasi waliyopata kwenye jamii na michango yao kwa taifa letu.
Mtemi Kibete alisahaulika kwa miaka mingi mpaka ilipofika mwaka 1976, wakati huo alikuwa na kama miaka tisini na nne; Mwalimu Nyerere alisafiri kwenda Tabora kumkabidhi nyumba mpya Mtemi Kibete Mwanamirambo, mmoja ya watoto wa Mtyela Kasanda, aliyejulikana zaidi kama Chifu Mirambo. Mtemi Kibete alikuwa ni mmoja ya watoto wa Chifu Mirambo waliokua hai mwaka huo.
Kibete alizaliwa mwaka 1882 na alifariki tarehe 25 mwezi was 12, mwaka 1982. Inasemekana alikuwa bado msichana mdogo wa miaka kumi na mbili baba yake, Chifu Mirambo, alipofariki mwaka 1894. Mtemi Kibete alikuwa mmoja ya watoto saba waliozaliwa na mama mmoja. Baba yake alikuwa na wake wengi walioka katika maboma yake matano, Isela, Meta, Ikonogo, Ukerebe, na Kiburuga. Kibete aliishi na mama yake katika boma la Isela homa.
Boma la Isela lilikuwa na ulinzi mkali. Chifu Mirambo aliweka askari wake hodari waliojulikana kama Warugaruga kulinda boma hilo na maboma yake mengine. Chifu Mirambo alikuwa anahama mara kwa mara kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Alikuwa anaenda boma la Isela na kukaa hapo kwa kama mwezi mmoja kila mwaka. Chifu Mirambo alikuwa anawapenda sana watoto wake. Alikuwa anacheza na Kibete na watoto wake wengine alipoenda kwenye boma lake la Isela. Alikuwa anacheza nao na kuwapa watoto wake wote upendo mkubwa. Hili alilisema Mtemi Kibete baadae. Wavulana wote walichukuliwa walipofika umri fulani na walipelekwa kujiunga na jeshi.
Mtemi Kibete alipewa bangili za shaba alizipata kama urithi kutoka kwa baba yake. Bado alikuwa na bangili hizo mwaka ilipofika akiwa na miaka kama tisini na nne. Hizo bangili za shaba zilitengenezwa na Watusi. Mtemi Kibete alipata kuwa Chifu wa kabila lake kwa kipindi kifupi kabla hajaondolewa na Waingereza. Mtemi Kibete alisahaulika kwa miaka mingi mpaka Mwalimu Nyerere aliposikia kuhusu taabu anazopata mwaka 1976 na uamuzi ukafanywa ajengewe nyumba.
Kibete alipata shida sana kipindi cha utawala wa Wajerumani. Wajerumani walituma wanajeshi waende kuvunja ofisi ya chifu wa Wanyamwezi. Wajerumani walipofika Ulyankulu wakamkuta Chifu Katunga, kaka yake Mtemi Kibete. Chifu Katunga alikuwa anapatana sana na mmoja ya wakoloni waliemwita Bwana Mzuri. Hakupatana kabisa na mkoloni mwingine aliyejulikana kama Bwana Toronto. Mama yake Mtemi Kibete alikuwa mjasiri sana. Siku moja alitofautiana na mama mmoja alieitwa Machunija. Machunija alikuwa rafiki wa Mabruku, aliyetumwa Tabora na Sultani Said Barghash kutoka Zanzibar. Mama yake Mtemi Kibete alimpiga Machunija. Mabruku akaenda kumshitaki kwa Wajerumani.
Mama yake Mtemi Kibete alikimbia na kujificha Kwande. Wajerumani wakamuamuru Chifu Katunga amkamate mama yake Kibete. Katunga akakataa. Bwana Toronto akaja na askari wake Ulyankulu. Askari waliwapiga risasi kaka watatu wa Mtemi Kibete, Maswa, Kihana, na Kapaya na kuwaua hapo hapo. Zaidi ya Wanyampala mia nne walikamatwa. Wengine sitini wakakamatwa, wote walifungwa na minyororo na kupelekwa geraza la Wajerumani Tabora. Bwana Toronto aliamua kuwaadhibu familia yote ya Chifu Katunga. Askari walichukua bunduki zote, ng’ombe wote walioweza kuwapata, pembe za ndovo zilizomilikiwa na familia na wakachoma moto vijiji vitano. Katika heka heka hizo, Watusi walikuja na kuchukua ng’ombe wote waliobaki wakaondoka nao.
Mtemi Kibete na kaka yake Chifu Katuga na wake zake wawili walienda Uha. Askari wa Kijerumani walikuwa wanawafuata wakijaribu kumkamata Katuga mpaka walipofika Lukela. Watu wengi kwenye kundi lao waliuliwa. Safari hio ya kuwakimbia Wajerumani ilikuwa ngumu sana. Walipata shida sana kupata maji. Njia moja ya kupata maji ilikuwa ni kufuata aina fulani ya ndege waliojua wapi pa kupata maji. Walitumia bunduki moja ya Chifu Katuga kuwinda wanyama kwa chakula. Walikuwa wanaweka kambi kwa siku tatu wakitafuta maji, kama kulikuwa hamna maji, basi waliendelea na safari yao. Pia walikuwa wanakula matunda waliyopata porini. Watu wengi walikufa kwa njaa katika msafara wao.
Kibete bado alikuwa mdogo. Kuna wakati Chifu Katuga ilibidi ambebe Kibete mgongoni wakati wanasafiri. Afya ya Kibete ilikuwa imezoofika sana. Katuga alihakikisha Kibete alikuwa na maji kidogo, ingawa wengine wengi walikuwa hawana maji. Uamuzi huo ulifanya baadhi ya watu kwenye msafari kuamua kuondoka na kwenda kwingine. Walisafiri kwa mguu mpaka Mana za Mlole, sehemu iliyokuwa inatawaliwa na Watusi kipindi hicho. Chifu wa Watusi aliwakaribisha wote na kuwapa chakula na sehemu ya kukaa.
Bwana Toronto akaja na mpango mwingine wa kumkamata Chifu Katuga. Alituma ujumbe kwa Katuga kumuomba warudi Ulyankulu na kwamba atawajengea kijiji kipya. Katuga na watu wengine 80 walikamatwa na Wajerumani walipofika Bunampanda wakati wakijaribu kurudi Ulyankulu. Mama yake Kibete pia akamatwa Kwande alipokuwa amejificha. Wajerumani walipanga kumnyonga Katuga, mama yake, na wafuasi wake wengine. Kwa bahati nzuri Bwana Mzuri aliekuwa safarini akarudi. Akafanya uamuzi wasinyongwe na wapelekwe Dar es Salaam. Chifu Katuga akaishi Dar es Salaam kama mkulima wa minazi mpaka alipokufa.
Chifu Katuga alimtuma Kibete na wengine warudi Ulyankulu akiwa Dar es Salaam. Walipofika nyumbani wakamkuta Kaibuka amepewa Uchifu. Hawakupatana kabisa na Kaibuka, wakaamua kwenda Tabora na kudai haki yao kwa viongozi wa kikoloni. Walipofika Tabora walifanikiwa na Mtemi Kibete akapewa uchifu. Hili lilikuwa jambo la kijasiri sana wakati huo. Kaibuka alikuwa anasaidiwa sana na wamisionari na wakoloni walikuwa wanataka yeye awe kiongozi. Mtemi Kibete alikuwa kiongozi wa nne kushika madaraka tangu Chifu Mirambo alipofariki. Waingereza hawakutaka kabisa Mtemi Kibete awe Chifu. Wakafanya njama za kumtoa na wakafanikiwa baadae
Mtemi Kibete aliolewa na Kigao, mtoto wa Chifu Ntinginya wa Usongo na Nyawa. Alifanikiwa kupata watoto watatu, wavulana wawili na msichana mmoja. Alikuwa na wajukuu 15 na watukuu 6 mwaka 1976. Aliishi kwa miaka 6 zaidi mpaka alipofariki mwaka 1982 akiwa na kama miaka mia moja na mbili.
Maisha ya Mtemi Kibete yanatupa nafasi nzuri ya kupitia tena historia ya Tanzania. Kuna wengi wametoa mchango mkubwa wakati wa harakati za kupambana na wakoloni. Wachache sana kama Mtemi Kibete wanatambulika kwa mchango wao. Mtemi Kibete ni mfano mzuri wa kuonyesha kwamba wakina mama walipata nafasi za uongozi na walitoa mchango wao mkubwa kwa jamii.
© Azaria Mbughuni
azmbughuni@gmail.com
Mei 7, 2019
Chanzo: Kanyama Chiume, “Surviving Daughter Mtemi Kibete Speaks”