Tuesday, August 28, 2018

Mapambano Kati ya Dossa Aziz na Zuberi Mtemvu Katika Uchaguzi wa Bagamoyo Mwaka 1960 na 1962

Dossa Aziz na Zuberi Mtemvu ni watu wawili waliotoa mchango mubwa kujenga TANU tangu chama hicho kilipoanzishwa mwaka 1954. Viongozi hawa wawili walishiriki kikamilifu katika harakati za kugombania uhuru. Zuberi Mtemvu alijiuzulu TANU na akaanzisha chama chake Tanganyika African National Congress (TANC) mwaka 1958. Moja ya sababu kubwa zilizofanya Mtemvu kugongana na viongozi wa TANU ilikuwa ni sera za kushirikiana na watu wa rangi tofauti kwenye uchaguzi. Dossa Aziz na Zuberi Mtemvu walipambana kugombea jimbo la Bagamoyo mwaka 1960. Huu ulikuwa kama mtihani kuona nani alikuwa na uvutio mkubwa kwenye siasa. Wagombea wote wawili walitumia muda mwingi kufanya kampeni na kuelezea sera zao kwa wakazi wa Bagamoyo. Uchaguzi wa Bagamoyo ulifanyika mwezi wa nane mwaka 1960. Katika uchaguzi huo, Dossa Aziz alipata kura 7,498 na Zuberi Mtemvu alipata kura 67. Wakazi wa Bagamoyo waliweka msimamo wao wazi kuhusu nani walimkubali. Aziz alipata ushundi mkubwa. Huu haukuwa mwisho wa malumbano kati ya viongozi hawa wawili. Dossa Aziz alipewa nafasi ya kuwa Territorial Film Censor muda mfupi kabla ya uhuru, mnamo mwezi wa kumi na moja mwaka 1961. Aziz alikubali kazi hio kwa maelewano kwamba kazi hio haitakuwa na mshahara wa kawaida, atalipwa “honorarium.” Ikumbukwe kwamba tayari kulikuwa na sheria iliyokataza mfanyakazi yeyote wa serikali kupata zaidi ya mshahara mmoja. Kazi hio ilikuja kuleta matata na Dossa Aziz akatolewa kama mwakilishi wa Bagamoyo. Hili halikumfurahisha. Akaamua kugombania tena kitongoji cha Bagamoyo kwenye uchaguzi uliopangwa kufanyika mwezi wa pili mwaka 1962. Uchaguzi huu ulikuwa muhimu sana. Tanganyika ilikuwa imepata uhuru. Mwalimu Nyerere alishajiuzulu Uwaziri Mkuu na Rashidi Kawawa alikuwa ndio Waziri Mkuu. Kwa mara nyingine tena, Dossa Aziz na Zuberi Mtemvu walikutana tena ulingoni kupigania jimbo la Bagamoyo. TANU ilitaka kuhakikisha Dossa Aziz anashinda na Zuberi Mtemvu hashindi uchaguzi wa Bagamoyo. Chama kikaanda kampeni kubwa kumpigia debe Dossa Aziz. Waziri Mkuu Rashidi Kawawa na Mwalimu Nyerere walikwenda Bagamoyo na kuwaomba wakazi wa Bagamoyo kumpigia kura Dossa Aziz. Viongozi wengine wengi wa ngazi ya juu walienda Bagamoyo kuwaomba wakazi wake wampigie kura Aziz. Kwa mara nyingine tena wakazi wa Bagamoyo waliweka msimamo wao wazi katika kura walizopiga. Dossa Azizi alitangazwa kama mshindi kwa kupata kura 3,207 wakati Zuberi Mtemvu alipata kura 89. Wakazi wa Bagamoyo, kwa mara nyingine tena, walimpa Dossa Aziz nafasi ya kuwaongoza. Na ndio ilikuwa mwaka huo huo, 1962, muasisi mwingine wa TANU, Abbas Sykes, alipewa nafasi ya Regional Commissioner wa Pwani. TANU ilitaka kuhakikisha wenyeji wa Pwani wanashikilia maeneo hayo.

© Azaria Mbughuni
azmbughuni@gmail.com

No comments:

Post a Comment