Ku Klux Klan (KKK): Kikundi cha Magaidi Marekani
Ugaidi sio kitu kipya duniani. Katika historia ya binadamu kuna mifano mingi watu au kikundi cha watu wametumia imani zao kuhalalisha ukatili usio na kifani. Hakuna kikundi kilicho mwaga damu Marekani kama KKK (Ku Klux Klan). Nilipata nafasi ya kutembelea Pulaski, Tennessee, kuona pahali KKK iliundwa. Pulaski, Tennessee ni mji ambao kikundi hichi cha kigaidi, kikundi kilichopata sifa kubwa ya uuaji wa kikatili, ubakaji, ulipuaji mabomu na mambo mengine mengi ya kikatili, kiliundwa mnamo mwaka 1866.
Pamoja na kwamba zaidi ya miaka 150 imepita tangu KKK iundwe, uamuzi wa kutembelea mji na nyumba ambayo kikundi hicho kiliundwa haukuwa rahisi. Haikuchukua muda mrefu kuliona jengo ambalo wazungu wa kusini waliopigana vita vya mwaka 1861-65 kati ya Marekani ya Kusini na Kaskazini walikutana na kuamua kuanzisha kikundi chao. Moja ya sababu ya hivyo vita ilikuja kuwa utumwa. Mwanzoni watu wa kusini Marekani walitaka kuachiwa waamue wenyewe sera zao, pamoja na ya utumwa. Kwa upande wa Kaskazini, wao walikuwa wanataka kujaribu kupunguza utumwa. Vita vilipoanza mwaka 1861 ilikuwa kwasababu sehemu za kusini zilitaka kujitenga na Kaskazini wakaanza vita ili kuhakikisha nchi haigawanyika. Mwanzoni hata watu wa Kaskazini pamoja na raisi Abraham Lincoln hawakuwa na nia ya kuondoa utumwa. Nia yao ilikuwa ni kuhakikisha nchi inabaki moja. Baada ya kama mwaka mmoja wa vita, upande wa Kaskazini ukastuka kwamba wa kusini walikuwa wanatumia watumwa kujijenga kwenye vita na kwamba wanaweza kuwashinda kusini kama wakitangaza utumwa umekwisha kusini. Hilo Lincoln alitanganza mwaka 1863. Vita hivi havikuanza kwasababu ya utumwa tuu, ila utumwa ukaja kuwa sababu kubwa ya hio vita na chanzo cha ushindi wa kaskazini baadae.
Turudi kwa askari waliopigana upande wa kusini, mnamo mwaka 1866, karibu mwaka baada ya vita kuisha, kikundi cha watu walikutana kwenye ofisi ya kinyozi wakaunda KKK huko Pulaski, Tennessee. Kikundi hichi cha kigaidi kilitumia nguvu, vitisho, umwagaji wa damu kuhakikisha watu weusi wanaoishi kusini wanarudi karibu na utumwa ingawa utumwa ulisha katazwa kutokana na sheria mpya za nchi. Katika mkutano wao wa kwanza mkubwa uliofanyika Nashville, Tennessee, viongozi walikuja kutoka miji mingi ya kusini, pamoja na Generali Nathan Bedford Forrest, mkuu wa majeshi ya kusini wakati wa vita. Generali Forrest alipewa cheo cha Grand Wizard wa KKK, mkuu wa kwanza wa KKK.
Kati ya 1868 na 1870, KKK ilihakikisha watu weupe wanashika sehemu zote za kusini kwa kutumia mabavu. Hatuwezi kujua watu weusi wangapi waliuliwa kikatili kuhakikisha watu weupe wanashika tena Marekani ya kusini. Wanasiasa karibu wote kuanzia Majaji na wakuu wa polisi (sheriffs) wanaochaguliwa kwenye uchaguzi wote walikuwa wanachama wa KKK. Kulikua hakuna haki kwa mtu mweusi kuanzia polisi mpaka mahakamani. Walikuwa wanakuja mchana nyumbani kwa mtu, wanamchukua na kumuua wazi kikatili kwa visababu tafauti, kama mtu kamsalimia mwanamke mzungu au visababu vingine visivyo na msingi; cha muhimu, na nia yao kubwa, ilikuwa kuwatisha watu weusi wabaki chini.
KKK ilikuja kuwa na wanachama wengi zaidi mwanzo wa karne ya ishirini. Inasemekana walikuwa na wanachama zaidi ya milioni nne katika Marekani kipindi hicho. Wanasiasa wengi walikuwa wanachama wa wazi wa KKK hadi miaka ya 1920. Mmoja wao alikuwa ni Hugo L. Black, jaji wa mahakama kuu ya Marekani.
Ni vigumu kusema watu wangapi waliuliwa na KKK. Lakini kuna wanaosema watu 4000 waliuliwa na kikundi hicho. Ukweli hatutaujua, kwani kuna wengi zaidi waliuliwa na hamna aliyetoa ripoti. Kuna mauji ya kikatili ya mji mzima wa watu weusi Tulsa, Oklahoma 1921, mauaji ya Emmet Till Mississippi 1955, mauaji ya Medgar Evers, bomu lilioua watoto kanisani Birmingham, Alabama 1963, na mauaji ya Jason Smith Louisiana 2011, yote yalifanywa na wanachama wa KKK. Smith walimkuta ametolewa utumbo ingiwa wanasema alizama kwenye maji. Mateso na taabu walizopata watu weusi Marekani kwa sababu ya hawa magaidi ni vigumu kueleza ieleweke. Leo hii kuna wazungu wengi ambao bado wanafuata sera za KKK ingiwa wanajificha na sio rahisi kuwajua. Baadhi yao ndio wanaongoza hii nchi. Tafakari hawa watu wanaoendesha nchi hii wanaangaliaje watu weusi, Waafrika, na watu wengine wasio wazungu leo hii!
Nilipita na kupiga picha kwenye hilo jengo la KKK nikajiondokea Pulaski, Tennessee. Sina mpango wa kutembelea mji huo tena, labda nirudi kupigana vita dhidi ya ubaguzi wa rangi na unyanyasaji wa binadamu wenzangu. Hapo nitarudi na kusimama na mkono mmoja juu!
© Azaria Mbughuni
No comments:
Post a Comment