Saturday, April 29, 2017

Ushirikiano wa Malcolm X na Tanzania na Sababu zilizofanya Auliwe

Ushirikiano wa Malcolm X na Tanzania na Sababu zilizofanya Auliwe
Malcolm X aliuliwa tarehe 21 mwezi wa 2 mwaka 1965. Pichani Malcolm X anaonekana akiwa Dar es Salaam mwaka 64 na wanafunzi wa Marekani. Picha nyingine ni mwili wake ukiwa na matundu ya risasi kwenye moyo. Je kuna uhusiano wowote kati ya mauaji hayo na ushirikiano wake na Tanzania?
Kabla ya hajauliwa, Malcolm alianza kujenga urafiki mkubwa na Tanzania. Msafara wa Tanzania, wakati huo Tanganyika na Zanzibar, walimpa ushirikiano mkubwa OAU mwezi wa saba mwaka 64 huko Cairo. OAU ilimuunga mkono kwenye jitihada zake kupinga ubaguzi wa rangi nchini Marekani. Malcolm X alijenga ushirikiano na Tanzania kati ya mwezi wa saba mwaka 64 na mwezi wa pili mwaka 65. Uhusiano huo ulimleta Dar es Salaam mwezi wa kumi mwaka 64. Abdulrahman Babu kutoka Zanzibar ndio alikuwa chanzo kikubwa cha ushirikiano kati ya Malcolm X na serikali. Alipokuwa Dar es Salaam, Malcolm alifanya maongezi na viongozi mbali mbali wa serikali na chama. Alikutana na raisi Nyerere ikulu na kufanya maongezi ya karibu masaa matatu. Uhusiano huu kati yake na viongozi wa Tanzania uliendelea mwishoni wa mwaka 64. Maafisi wa upelelezi wa Marekani, FBI, walimfuata Malcolm mwezi wa 12 akitoka uwanja wa ndege New York ambapo walimuona akiwa na maafisi wa ubalozi wa Tanzania. Aliingia kwenye gari la maafisa wa ubalozi wa Tanzania na kuondoka kuelekea kwenye nyumba ya afisa mmoja wa ubalozi. Miezi miwili baadae aliuliwa kikatili. Kwanini? 
Ni kweli kwamba Malcolm alikuwa na ugomvi mkubwa na viongozi wa kundi la dini ambalo aliachana nalo mapema mwaka 64. Kuna wanaosema ugomvi huo ni moja ya chanzo cha kuuliwa. Ni kweli alipigwa risasi na watu wanaosemekama walikuwa kwenye kundi hilo la kidini; ingiwa hilo halijathibitishwa kikamilifu. Kuna wengi wanaamini aliuliwa na watu wa serikali. Hata hivyo, mtu pekee aliyeshikiliwa kwa kumuua Malcolm X, Thomas Hagan, aliachiwa jela mwaka 2010. Kitu gani kinaweza kufanya muuaji wa Malcolm X aachiwe huru kama serikali haina mkono? Picha ya mwili wa Malcolm X akiwa amekufa, inaonyesha matundu matatu ya risasi kwenye sehemu ya moyo; aliyefyatua risasi alikuwa na ujuzi mkubwa. Kuna maswahili mengi ambayo hayana majibu rahisi nani alimuua na kwasababu gani. Lakini ni wazi kwamba tangu alipotembelea Afrika mwaka 64 na alipoanza kujiunga na viongozi wa Afrika, Malcolm alikuja kuwa tishio kubwa kwa serikali ya Marekani. Harakati zake alipoenda kwenye mkutano wa OAU za kujaribu kushawishi nchi za Afrika zijaribu kusaidia mapambano ya watu weusi Marekani, zilianza kufanya kazi mwishoni wa mwaka 64. Nchi za Afrika zililaani vitendo vya Marekani kwenye mkutano wa umoja wa mataifa New York mwezi wa 12. Mashambulizi hayo dhidi ya Marekani huko umoja wa mataifa yaliiaibisha nchi hio. Hamna shaka kwamba juhudi za Malcolm X zilikuwa zinaanza kufanya kazi. Na ni kwasababu hio serikali ya Marekani ilianza kumuona yeye kama adui namba moja! 






No comments:

Post a Comment