Familia ya Sykes ni moja ya familia muhimu katika historia ya Tanzania. Kuanzia Abdulwalid Sykes, Abbas Sykes, na wengine katika familia kuna mengi yanasemwa kuhusu mchango wa familia ya Sykes katika kwa Tanganyika/Tanzania. Mengi zaidi yameandikwa kuhusu miaka ya hamsini, lakini pia kuna michango mingine ilifanywa miaka ya sitini ambayo haiongelewi. Moja ya michango iliyosahaulika ni katika uhusiano kati ya ASP ya Zanzibar na TANU.
Mnamo mwaka 1960, Mtoro Rehani na Eddy Kleist Sykes (dada wa Abbas and Abdulwalid), walihudhuria mkutano wa TANU kwa niaba ya ASP ambako kulifanyika maongozi ya uwezekano wa "Federation" (Ushirikisho) na "unification" (Muungano). Abbas Sykes alikuwa mmoja wa viongozi wa TANU aliyekuwa anapeleka ujumbe na pesa kwa ASP ya Zanzibar kati ya mwaka 1960 na 1963. Mwaka 1961 Abbas Sykes alienda Zanzibar na Ali Mogne Haloua na Roland Mwanjisi na kufanya mkutano wa siri na ASP. Abbas Sykes alitoa Shs. 7500 za TANU na kuwapa ASP. Pesa hizo zilitolewa kwa maelewano kwamba itakuwa siri. Mwaka 1962 Abbas Sykes alienda Zanzibar na kukutana na ZPFL. Aliwaambia ZPFL kwamba TANU itaacha kuwapa msaada kama wakiendelea kushambulia ASP. Abbas Sykes alienda Zanzibar mwanzoni wa mwaka 1963 na kuhudhuria mkutano wa ASP akiwa na ujumbe kutoka serikali ya Tanganyika. Waliokuwepo kwenye mkutano huo ni pamoja na Hassan Nassor Moyo na Ahmed Diria Hassan.
Kuna mahali nilisoma kwamba serikali ya Tanzania na TANU haikutaka kuandika mahali popote kuhusu mchango wa Abdulwalid Sykes. Katika utafiti wangu, nilikuta makala moja iliyoandikwa kwenye gazeti la serikali miaka ya sabini (Daily News) yenye kichwa cha habari "Sykes One of TANU Pioneers" yaani Sykes Alikuwa Mmoja ya Waasisi wa TANU." Makala hii inaongelea mchango wa Abdulwalid Sykes katika miaka ya hamsini. Haya ni baadhi ya mambo yaliyoandikwa katika makala hio iliyoandikwa kwa kiingereza.
Inasema: "Mr. Sykes was a founder member of Tanu. By his death the party lost one of its first pioneers. His political activities started way back before the formation of TANU. He was President of the Tanganyika African Association (TAA) from which TANU emerged."
As for the name TANU, the article asserts "..Mr. Abdul Sykes suggested the name of the new Party to be Tanganyika African Union (TAU). However his colleagues objected saying that it was very similar to Kenya African Union (KAU) that had already been banned by the colonialists. "They thought under such a name the colonialists would use the name as pretext to ban TAU. Mwalimu Nyerere then suggested that a word "National: be included, making the name Tanganyika National African Union. "Mr. Ally Sykes a brother of Abdul Walid objected to Mwalimu Nyerere's suggestion saying that the short form of the party name-TNAU-would not be easy to pronounce. He called for another arrangement of the words. This resulted into an acceptable party title-TANU."
Makala hii ya gazeti la serikali inasema kwamba Abdul Sykes alikuwa ni mmoja wa waasisi wa TANU, kwamba alikuwa kiongozi wa TAA kabla Mwalimu Nyerere hajachaguliwa kuwa mwenyekiti wa TAA, na inaongelea jinsi wanafamilia ya Sykes walivyochangia kuja na jina la TANU.
Ni wazi kwamba Tanganyika haikupata uhuru kwa mchango wa mtu mmoja na pia kuna wengi walijitolea katika miaka ya mwanzo baada ya uhuru kujenga nchi hii kama ilivyoandikwa na gazeti la serikali na nyaraka zingine zilizogusia mawasiliano kati ya Abbas Sykes na viongozi wa ASP. Kila mmoja alitoa mchango wake kwa Tanganyika/Tanzania, na pamoja, nguvu ya wananchi ilihakikisha ushindi katika harakati za kupata uhuru kutoka kwa mkoloni na kujenga nchi baada ya uhuru
Azaria Mbughuni
September 26, 2017